Sunday, March 30, 2014

Rais Kikwete aanza ziara Uingereza






RAIS Jakaya Kikwete amewasili mjini London, Uingereza, kwa ziara rasmi ya siku tatu ya kidola, moja ya ziara nadra kufanywa na viongozi wa nchi za nje nchini Uingereza.
Rais Kikwete na ujumbe wake aliondoka nchini Jumamosi kuelekea London kwa ziara hiyo ya siku tatu ambako atakuwa mgeni rasmi wa Serikali ya Uingereza.
Katika ziara hiyo, Rais Kikwete ambaye ameambatana na Mama Salma Kikwete, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe;Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo, Waziri wa Fedha Saada Mkuya na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Nassoro Mazrui.
Rais pia amefutana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Tekolojia, January Makamba.
Baada ya ziara ya Uingereza, Rais Kikwete atakwenda Brussels, Ubelgiji, kuhudhuria Mkutano wa nne wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Afrika - EU-Africa Summit - uliopangwa kufanyika kwa siku mbili - Jumatano na Alhamisi, kwenye Makao Makuu ya EU, mjini Brussels.
Mkutano huo ambao mada kuu itakuwa ni Umuhimu wa Kuwekeza katika Watu, Ustawi na Amani, utahudhuriwa na wakuu wa nchi wanachama wa EU na wale wa Afrika, akiwamo Rais Kikwete.
Mikutano ya wakuu wa nchi za EU na Afrika imefanyika mara tatu mpaka sasa kuanzia na ule wa kwanza wa mwaka 2000 mjini Cairo, Misri ukifuatiwa na ule wa Lisbon, Ureno mwaka 2007 na Tripoli, Libya mwaka 2010.
Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kuhudhuria mkutano huo tangu aanze kuongoza Tanzania mwishoni mwa 2005.
Rais Kikwete pia ameombwa kuhudhuria mikutano mingine kadhaa ambayo itafanyika wakati wa mkutano huo mkubwa.

src
Habari Leo