Saturday, March 1, 2014

MASHABIKI YANGA WAZUA BALAA BOKO




Ibrahimu Mussa
BAADHI ya mashabiki wa Yanga wamelalamikia kitendo cha uongozi wa klabu hiyo kutumia kiasi kikubwa kulipia uwanja ambao wanafanyia mazoezi klabu hiyo ya Boko Veterani kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, kwa madai kuwa wana uwezo wa kujenga wa kwao.
Mashabiki hao walikuwa wakifuatilia mazoezi hayo na kushuhudia namna uwanja huo ulivyo na ‘pichi’ nzuri, hali ambayo pia ilionekana kuwafurahisha wachezaji wa timu hiyo. Yanga hulazimika kutoa shilingi 350,000 kila siku kwa ajili ya malipo ya uwanja huo kitendo ambacho mashabiki wanapinga na kudai ni vema wakajenga uwanja wao.
Mmoja wa mashabiki hao aliyefahamika kwa jina la Moses Kenyata, alihoji kama timu yao ina uwezo wa kusajili wachezaji wenye majina makubwa kwa nini wanashindwa kuweka nyasi katika Uwanja wa Kaunda! “Huu uwanja unamilikiwa na watu binafsi wenye mapenzi na mchezo wa soka, lakini timu yetu ya Yanga inashindwa kuwa hata na uwanja kama huu wakati tuna uwezo wa kusajili wachezaji wenye majina makubwa. “Kama leo (jana) mashabiki tumeacha kazi zetu kuja kuishuhudia timu yetu hapa, ambao tuna uwezo wakuchangishana hata shilingi 5,000 kwa kila mmoja wetu kupitia katika matawi yote hapa nchini,” alisema Kenyata.