Wednesday, March 26, 2014

KUELEKEA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA MUUNGANO: Serikali tegemezi na egemezi haiwezi kuwa mhimili wa Muungano

MWEZI ujao, nchi yetu inaadhimisha miaka 50 ya Muungano huku Bunge Maalum la Katiba linaloketi Dodoma likuwa na kibarua, pamoja na mambo mengine, kupitisha Katiba mpya ambayo itaimarisha Muungano wetu kwa miaka 100 na zaidi ijayo.
Wiki iliyopita Rais Jakaya Kikwete alilihutubia Bunge hilo na kuwasihi wabunge kusoma na kutafakari kwa kina juu ya pendekezo la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa muundo wa serikali tatu ili kuepuka kuunda Katiba itakayoyumbisha Taifa kisiasa na kiuchumi.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alirejea Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba Jaji Joseph Warioba ambayo pamoja na mambo mengine, inapendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali Tatu ambazo ni Serikali za Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika.
Rasimu hiyo imeundwa kwa kuzingatia maoni ya wananchi ambapo kinadharia yanaonekana kupatia ufumbuzi wa kero za Muungano ambao mwezi ujao utatimiza umri wa miaka 50. Rais Kikwete ambaye amekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa takribani miaka tisa sasa ametumia uzoefu wake wa utekelezaji wa shughuli za Muungano kueleza changamoto na udhaifu wa muundo wa Shirikisho wa Serikali Tatu.
Kikwete anasema bila kipato cha uhakika na msingi imara itakuwa vigumu kwa Serikali ya Muungano inayopendekezwa kutekeleza majukumu yake kwa uhakika kwa sababu vyanzo vyake vya mapato si vya uhakika. Anabainisha kuwa Serikali tegemezi na egemezi haiwezi kamwe kuwa mhimili na nguzo ya kuimarisha Muungano badala yake inaweza kuudhoofisha, jambo ambalo asingependa litokee bila kuweka angalizo.
Kikwete anasema kwa mujibu wa Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano imepewa fursa ya kukopa kama chanzo cha kujipatia mapato ya kuendesha shughuli zake. Hata hivyo, serikali hiyo inaweza kukosa sifa za kukopa kutokana na kukosa rasilimali zake yenyewe.
Katika mfumo wa Serikali Tatu unaopendekezwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba, masuala yanayohusu uchumi na maendeleo ya jamii kama vile kukuza kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, biashara, pembejeo, elimu, na hifadhi yako chini ya mamlaka ya Serikali za nchi washirika na kimsingi Serikali ya Muungano haina mamlaka ya kuingilia mambo yanayohusiana na rasilimali za nchi washirika.
Mamlaka ya Serikali ya Muungano inapaswa kushughulikia mambo saba ambayo ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa na jambo la saba ni Ushuru wa bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Kwa mujibu wa Rasimu ya Katiba aya ya 231 Serikali ya Muungano ina vyanzo vitano vya mapato ambayo ni ushuru wa bidhaa, mapato yasio ya kodi yanayotokana na taasisi na taasisi za Muungano, michango kutoka kwa Nchi Washirika ikiwa na maana Tanganyika na Zanzibar, mikopo kutoka ndani na nje ya Muungano na mapato mengine.
Uchambuzi uliofanywa na Profesa Issa Shivji kuhusu utatanishi na Ukimya katika Rasimu ya Katiba mpya unaonesha kuwa rasimu haijaweka wazi juu ya ushuru wa bidhaa jambo linaloweza kuleta utata kwa kuwa haielezwi wazi kama ni ushuru wa bidhaa unaosimamiwa na Idara ya Forodha kwa maana ya excise duty au ushuru wa kodi kama wa ongezeko la thamani (VAT), sales tax ama produce cess.
Shivji anasema utata huo unaweza kuzua mgogoro katika utekelezaji wake na hasa ikizingatiwa kuwa Serikali ya Muungano haisimamii rasilimali za nchi washirika. Shivji anasema Rasimu ilitakiwa kutoa ufafanuzi zaidi juu ya ushuru huo kwa sababu ushuru wa bidhaa unakusanywa mahali pa uzalishaji, uuzaji na ulaji.
Kwa mujibu wa rasimu ya Katiba inaelekea ushuru wa bidhaa ndio utakuwa chanzo kikuu cha Mapato ya Serikali ya Muungano wakati kuna idara moja tu katika mambo ya Muungano ambayo inaweza kutoa mapato haya, nayo ni uraia na uhamiaji.
Shivji anasema ingawa inaonekana kuwa usajili wa vyama vya siasa pia unaweza kutoa mapato jambo hilo pia lina utata kwa kuwa katika muundo wa serikali tatu chama cha siasa kinaweza kuamua kugombea uchaguzi eneo moja la Muungano, Tanganyika au Zanzibar ama katika ngazi ya Muungano.
Endapo chama kitaamua kugombea sehemu moja ya Muungano kinaweza kukataa kulipa ada katika Serikali ya Muungano. Serikali ambayo haina chanzo chake huru cha mapato au sekta ya uzalishaji au walipa kodi wakubwa, hususan mashirika, chini yake, itakuwa na hali ngumu ya kupata mikopo. Kwa jumla, Shivji anasema kuna utatanishi na wasiwasi kwa upande wa mapato ya Muungano.
Ni wazi kwamba kuendesha Serikali ya Muungano kutakuwa na gharama kubwa kwa kuwa kazi inayofanywa na taasisi moja au idara moja katika muundo uliopo sasa itahitaji taasisi mbili. Uchambuzi huo wa Shivji unaendana na mtazamo wa Rais Kikwete ambaye anasema kuwa katika muundo wa Serikali tatu, Serikali ya Muungano itakosa nguvu ya kutekeleza majukumu yake.
“Kwa jumla hii ni Serikali ambayo ukuu wake hauna nguvu iliyo thabiti, na watu wengine wanaona kama vile ukuu huo haupo kabisa,” anaeleza Kikwete.
Anatoa mfano kuwa endapo atatokea kiongozi yeyote wa nchi washirika atatunisha misuli dhidi ya Rais wa Muungano au kupinga maamuzi ya Serikali au chombo cha Muungano, Rais wa Muungano na Serikali yake hawatakuwa na lo lote la kufanya kwa maana ya kwamba ‘watafyata mkia’.
“Kwa kweli uhai wa Muungano katika muundo wa Serikali tatu ni wa mashaka makubwa,” Kikwete anasisitiza. Hofu kuhusu udhaifu wa Serikali ya Muungano chini ya mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa, inawasumbua hata wale wanaopendelea mfumo wa Serikali Tatu kwa kuwa azma yao ni kuwa na Serikali ya Muungano yenye nguvu na inayoweza kusimamia mambo ya Muungano bila kubabaika.
Jambo lingine linalotia shaka katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali ya Muungano ni kifungu cha 229 kinachoibebesha Serikali ya Muungano mzigo wa madeni kutoka Nchi Washirika. Kwa mujibu wa rasimu kifungu 229 (1) Serikali ya Nchi Mshirika itakuwa na mamlaka ya kukopa fedha ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kugharimia shughuli zilizo chini ya mamlaka ya Muungano.
(2) Endapo mkopo unahitaji dhamana, Serikali ya Jamhuri ya Muungano, baada ya kushauriana na kukubaliana na Serikali za nchi Mshirika, inaweza kutoa dhamana kwa mkopo ulioombwa. Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya uchumi wanahoji ni vipi serikali isiyokuwa na rasilimali wala uzalishaji inaweza kudhamini mikopo ya nchi Washirika?
Endapo nchi Mshirika atachelea kulipa deni, Serikali ya Muungano itapata wapi uwezo wa kulipa wakati yenyewe inategemea mchango kutoka kwa nchi Washirika? Ni dhahiri kuwa mfumo huo wa Serikali Tatu hautaweza kuimarisha Muungano ikiwa Serikali ya Muungano inayopaswa kuwa na mamlaka ya juu itakuwa tegemezi na ombaomba kwa serikali za nchi washirika.
Shivji ameainisha pia utatanishi kuhusu wajibu wa Benki Kuu na kudai kuwa muundo wa serikali tatu imedhoofisha majukumu ya Benki Kuu ya Muungano, hali inayoweza kusababisha uchumi wa nchi kuyumba.
Anasema Benki Kuu ina nafasi kubwa katika kudhibiti uchumi kwa kuwa fedha na mzunguko wa sarafu na uhamishaji wa fedha unakuwa na nafasi katika Uchumi unaotegemea uuzaji na ununuaji wa bidhaa ya kipekee kwa kuwa akiba inawekwa kupitia fedha; uwekezaji unahesabiwa kwa fedha; rasilimali zinathaminiwa kwa fedha.
Benki Kuu ni taasisi nyeti inayosimamia fedha katika sura zake mbalimbali. Majukumu muhimu ya Benki Kuu ni kutoa na kusimamia sarafu na fedha na mzunguko na uhamishaji wake; kusimamia ujazi wa fedha (money supply) na amana (bank deposits) katika benki zote pamoja na za kibiashara.
Pia Benki Kuu ina wajibu wa kutunga na kusimamia sera ya kifedha; kuratibu, kudhibiti na kuhakiki mabenki ya biashara na uwekezaji katika nchi; kudhibiti mfumuko wa bei, ikiwemo bei ya fedha za kigeni; na hatimaye ni benki ya serikali. Kwa muhtasari, Benki Kuu ni mtunzaji, mlinzi, mwangalizi na msimamizi wa fedha za taifa pamoja na akiba ya nchi, ikiwa ni pamoja na akiba ya dhahabu au fedha za kigeni.
Shivji anasema ili kunusuru Taifa lenye uchumi duni Benki Kuu inapaswa kudhibiti na kuongoza soko, badala ya kufuata soko. Benki Kuu ikifuata soko bila kuwa na msimamo kwa mujibu wa sera ya fedha, na mtazamo wa maendeleo wa nchi, itakuwa kama bendera inayopepea kwa kuelekezwa na upepo badala ya kudhibiti mwelekeo wa upepo.
Anasema Benki Kuu inatakiwa kuwa kinu kinachonasa upepo ili kujijengea nguvu, sio bendera inayoyumbishwa na upepo na kwamba nchi haiwezi kuwa na benki kuu zaidi ya moja. “Kwa vyovyote vile, huwezi kuwa na Benki Kuu zaidi ya moja katika nchi moja hata kama ni nchi ya shirikisho,” Shivji anaeleza.
Anasema ingawa Benki Kuu ni jambo la Muungano kuna tofauti kati ya vipengele vilivyoko kwenye Katiba ya sasa na Rasimu ya Katiba mpya na kudai kuwa vipengele vilivyoko kwenye rasimu ni dhaifu ikilinganishwa na vilivyoko kwenye Katiba ya mwaka 1977 ambayo inafanyiwa mabadiliko.
Rasimu inasema, ‘Sarafu na Benki Kuu’ ni jambo la Muungano. Jambo ambalo ni tofauti na Katiba iliopo inayosema kwamba, ‘Mambo yote yanayohusika na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yote halali ikiwa ni pamoja na noti ni mambo ya Muungano. Pia Katiba ya sasa inasema Benki Kuu inahusika na benki za kuweka akiba na shughuli zote za mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni ni jambo la Muungano.
Vipengele vilivyoko kwenye Katiba vina maana pana zaidi, kwa kuwa Katiba inataja sio sarafu tu bali mambo yote yanayohusika na fedha, ikiwamo, sera za kifedha pamoja na hayo inataja usimamizi wa fedha za kigeni.
Rasimu inazipatia benki za Washirika nguvu kubwa kama inavyoonekana kwenye Ibara 233 kuwa Washirika wanaweza wakawa na benki zao zitakazokuwa na jukumu la kutunza akaunti ya fedha za serikali husika, kusimamia Sera za Kifedha na benki za biashara katika mamlaka zao.
Majukumu ya Benki Kuu yaliyotajwa katika Rasimu ni manne kwa mujibu wa ibara ya 233 (a) kutoa sarafu, kudhibiti na kusimamia mzunguko wa sarafu; (b) kuandaa na kusimamia Sera na mipango inayohusiana na sarafu; (c) kudhibiti na kusimamia masuala ya fedha za kigeni; na (d) kusimamia Benki za Washirika wa Muungano yaani Benki za Tanganyika na Zanzibar.
Shivji anasema Aya (a) na (b) hazina shida kwa sababu zinahusika na sarafu ambayo ni jambo la Muungano. Lakini aya (c) na (d) sio mambo ya Muungano kwa mujibu wa Rasimu hiyo.
Kwa kuwa masharti ya Katiba ya Shirikisho, ambayo hayahusiki na mambo ya Muungano, hayawabani Washirika, inawezekana kabisa Washirika wasitilie maanani aya hizo na kufanya shughuli zao kupitia benki zao jambo ambalo linaonesha wazi Serikali ya Muungano itazidiwa nguvu na Serikali za nchi Washirika.
Ni matumaini ya Watanzania wengi kwamba Bunge Maalum litafanyia kazi mawazo yanayoona hofu ya pendekezo la serikali tatu kuwa inaweza kuwa sababu ya kuvunja Muungano na kuyafanyia kazi.

src
Habari Leo