Thursday, March 27, 2014

Katiba Mpya ya 2015 au ya 2115?

 
TANZANIA inapita katika kipindi muhimu cha historia ya uhai wake na kwa mara ya kwanza tokea kuanzishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi imeundwa Tume ya Rais ya kukusanya maoni kuhusu aina ya katiba wanayoitaka wananchi.
Tume hiyo iliyoongozwa na waziri mkuu na makamu wa pili wa rais wa zamani Jaji Joseph Sinde Waryoba, iliundwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Aprili 6, 2012. Pamoja na kuwapo makundi yanayopinga baadhi ya mambo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba mpya ambayo Jaji Waryoba aliiwasilisha rasmi Bungeni wiki iliyopita upingaji ule hauchuji wala kuondoa mambo mengi mazuri na ya msingi yaliyomo mle.
Lengo la kurejea kwa safu hii katika kipindi hiki ni kutoa mfululizo wa mawazo yangu, nikiwa mwanataaluma wa mambo ya habari na mawasiliano, kama mchango wangu kwa wajumbe wa Bunge la Katiba pale wanapoelekea kuanza kuipitia Rasimu ya Katiba na kujadili ni yapi ya msingi yabaki na yapi yanahitaji marekebisho.
Nikiri mapema tu kwamba sehemu ya mawazo haya yanatokana na makala niliyoandika Novemba 2012 kwa ajili ya Kituo cha Demokrasia nchini (TCD) ambacho kiliandaa mchango wake wa makala za kitaalamu na kuukabidhi kwa Tume ya Warioba.
Katika wakati ule nilipata pia fursa ya kufanya utafiti miongoni mwa waandishi wa habari wenzangu juu ya nini walichotarajia katiba mpya iseme kuhusu sekta ya habari na mawasiliano ya umma kwa ujumla.
Lakini pia ninanawirisha mawazo yangu kwa kurejea tafiti na nadharia mbalimbali za wataalamu kadhaa duniani. Safiri nami katika mfululizo wa makala haya na tusaidiane katika kustawisha mjadala wa wazi kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa katiba bora katika nchi yetu.
Kwa mujibu wa Profesa Mwesiga Baregu (2000) mfumo wa uandikaji katiba tokea uhuru mwaka 1961 umekuwa wa kuweka viraka viraka. Anasema pamoja na mapendekezo muhimu ya Tume ya Jaji Francis Nyalali (1992) kuhusu namna ya kuimarisha demokrasia ya vyama vingi, na baadaye mapendekezo mengine ya Jaji Robert Kisanga (1998) kumekuwa hakuna utashi wa kisiasa kuhakikisha katiba inaaandikwa upya kukidhi mahitaji ya demokrasia ya vyama vingi.
Wanazuoni na wataalamu wa masuala ya katiba kama Profesa Issa Shivji ambaye ni Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamesisitiza kuwa fursa iliyopo ya kuunda upya katiba itumike kuandika katiba ambayo itaakisi matakwa ya wananchi.
Madhumuni makuu ya makala haya ni kutoa mapendekezo ya sekta ya habari kuhusu ulinzi na uwajibikaji wa vyombo vya habari kwenye Katiba mpya. Lakini mapendekezo yenyewe hayana budi kutokana na muktadha wa historia, maana ya dhana na mahitaji ya wakati ya taifa letu kwa sasa.
Ni kwa mantiki hii basi makala haya yanatoa muhtasari wa historia ya nafasi ya vyombo vya habari katika katiba ya Tanzania na dhima viliyokabidhiwa tokea nchi ilipopata uhuru mwaka 1961. Makala haya pia yanajadili kwa muhtasari mawazo ya wanazuoni kuhusu dhima ya vyombo vya habari katika demokrasia – kwa kuzingatia kwamba Tanzania ni nchi inayofuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.
Kadhalika, makala haya yanajadili kwa muhtasari mahitaji ya vyombo vya habari katika demokrasia ya Tanzania hasa kwa kuzingatia hali halisi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ilivyo na hatimaye kuwasilisha matokeo ya maoni ya wahariri, wanazuoni na wadau wengine kuhusu matarajio yao katika Katiba mpya.
Mwisho makala haya yanawasilisha mapendekezo yanayotokana na udadavuzi na uchambuzi wa machapisho na nadharia kuhusu dhima ya vyombo vya habari katika demokrasia, na pia mawazo ya wadau waliohojiwa kuhusu ulinzi na uwajibikaji wa vyombo vya habari nchini.
Historia Tupi ya Vyombo vya Habari Tanzania
Historia ya vyombo vya habari Tanzania (Tanganyika) inaweza kugawanywa katika vipindi vinne (rejea pia Mfumbusa 2006; Rioba 2012). Kwanza ni kipindi cha vyombo vya mawasiliano kabla ya kuja kwa wageni wa kilowezi na wakoloni. Pili ni kipindi cha wamissionari na baadaye wakoloni kuanzia miaka ya 1800. Tatu ni kipindi baada ya uhuru kuanzia mwaka 1961. Nne ni kipindi baada ya kurejeshwa mfumo wa vyama vingi vya siasa miaka ya 1990.
Vyombo vya mawasiliano na habari kabla ya wageni
Falsafa: Mawasiliano kama sehemu ya maisha
Wanazuoni mbalimbali (rejea Ugboajah 1985, Bourgault 1995, Shaw 2009, Rioba 2012) wameelezea kwamba nchi za Afrika zilikuwa na mifumo yake ya mawasiliano na kupashana habari ambayo ilitumika kutekeleza dhima ya vyombo vya habari katika jamii hizo. Falsafa kuu ya mawasiliano wakati ule ilikuwa: Mawasiliano kama sehemu ya maisha. Na dhima kuu ilikuwa ni (i) kuhabarishana (ii) kufunzana (iii) Kujadiliana (iv) kuibua maovu (v) kukosoana  (vi) kuburudishana. Na kwamba njia kuu za kutimiza dhima hii zilikuwa: (i) wakwezi walipanda miti au miamba mirefu kuchunguza kulikoni na kuhabarisha umma.
Walitumwa pia wapeleke ujumbe wakizunguka katika jamii wakipiga mbiu na kutoa taarifa kuhusu jambo lolote lenye maslahi kwa umma (ii) kulikuwa na tamaduni kama za jando na unyago zilizotumika kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu wajibu wao katika jamii.
Kulikuwa pia na babu na bibi waliokuwa wakitoa hadithi zenye mafunzo kwa watoto na vijana kuhusu tabia na mienendo iliyotukuka. Kulikuwa na wataalamu wa masuala mbalimbali waliotoa mafunzo kwa wengine katika jamii ili kuwezesha utaalamu ule kuendelea kusaidia jamii zaidi kwa vizazi na vizazi; (iii) wanajumuiya walikutana pahala maalumu kwa ajili ya majadiliano kuhusu masuala mbalimbali yaliyohusu maisha yao; (iv) kulikuwa na wasanii wa kughani (kama alivyo Mrisho Mpoto) ambao kazi yao ilikuwa ni kuchunguza (au kuelezwa na wanajamii) mambo yaliyoenda kinyume na maslahi ya jamii na wakayatungia mashairi.
Kila walipoimba mashairi yale kwa njia ya kukanya au kuaibisha wakosaji katika jamii ujumbe ulifiwafikia wahusika hata bila ya kutajwa majina; (v) walikuwapo wapiga zeze, litungu, mbegete, zumari, ngoma, maigizo, ngonjera, nyimbo, michezo kama vile mieleka, kukimbia, n.k. kwa ajili ya kuburudisha jamii; (vi) lakini zaidi ulikuwapo mfumo wa kimawasiliano uliohakikisha kwamba kunakuwapo na amani, utangamano, mshikamano na uimara wa jamii. Wote walioshiriki kwa njia moja ama nyingine katika shughuli za mawasiliano haya walitambuia uwajibikaji wao kwa jamii uliotokana na kanuni za maadili ya jumuiya.
Vyombo vya habari vya wamisionari/wakoloni        
Falsafa: Mawasiliano kama sehemu ya kustaarabisha wenyeji
Wamisionari walipoingia Tanganyika na Zanzibar walianzisha vyombo vyao vya habari kwa ajili ya kutekeleza dhima ya mahitaji yao katika bara hili. Na hata walipokuja wakoloni vyombo vya habari viliendelea kufanya kazi ile ile ambayo wamisionari walikwishaianzisha.
Kwa mfano, inajulikana kwamba gazeti la kwanza la kimisionari kuanzishwa hapa Afrika Mashariki lilikuwa Msimulizi (lilianzishwa Zanzibar mwaka 1888) kwa ajili ya wamisionari (Rioba 2009). Kwa muhtasari tu dhima ya vyombo vya habari vya wamisionari na wakoloni ilikuwa: (i) kuhabarisha wamisionari wenzao na walowezi kuhusu matukio ya nyumbani kwao Ulaya; (ii) kutukuza imani yao na ustaarabu wao na kubeza tamaduni za Kiafrika; (iii) Kuwezesha mawasiliano ya serikali ya kikoloni na watawaliwa; (iv) kufundisha wenyeji mila, desturi na utamaduni wa Magharibi; (v) kutoa burudani kwa wageni na wenyeji; (vi) kuwezesha kuunganisha uchumi wa makoloni na wakoloni (rejea Rioba 2012).
Lakini katika suala la uwajibikaji, wakoloni waliweka sheria kali kudhibiti vyombo vya habari vya wenyeji dhidi ya kile walichokiita uchochezi (angalia Sturmer & Rioba 2000, Sturmer 2000). Haikuwa ajabu basi kwamba mmoja wa waathirika wakuu wa sheria zile alikuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa mhariri wa gazeti la wazalendo la Sauti ya TANU ambalo lilikuwa sauti ya wapigania uhuru.
Mwalimu Nyerere alishitakiwa na wakoloni kwa kosa la uchochezi alilotuhumiwa kulitenda kupitia Sauti ya TANU. Vyombo vya wamisionari na vile vya wakoloni vilijidhibiti vyenyewe lakini kwa kuzingatia falsafa, matakwa na maslahi ya wakoloni (rejea Sturmer & Rioba 2000). Jambo muhimu la kuzingatia katika kipindi hiki ni ukweli kwamba vyombo vya habari vya wazalendo vilipigwa vita kwa sababu vilitishia maslahi ya watawala kwa kuwaamsha wananchi walio wengi kuhusu haki zao.
Vyombo vya habari baada ya uhuru
Falsafa: Mawasiliano kwa ajili ya kujenga nchi
Baada ya uhuru mwaka 1961 serikali ya Tanganyika ilianza kuchukua hatua kadhaa kuhakikisha inarejesha heshima ya wananchi wake waliokuwa wameonewa, wamenyonywa na kupuuzwa kwa miaka mingi ya utumwa na ukoloni (rejea Azimio la Arusha 1997).
Hivyo basi kufikia mwaka 1964 Tanganyika na Zanzibar zikaungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu za kijiografia, lakini pia kutokana na historia ya nchi hizi kuwa na watu waliokuwa wameingiliana sana.
Mwaka 1967 serikali ya TANU ikaleta Azimio la Arusha lililolenga kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi unakuwa mikononi mwa umma. Kutokana na falsaha ya Azimio la Arusha iliyolenga kuweka njia kuu za uchumi mikononi mwa umma dhima ya vyombo vya habari ilibainishwa upya.
Mwaka 1970 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere akaja na sera mpya ya gazeti la The Standard ambalo lilibadilishwa na kuitwa The Daily News. Sera mpya ikiongozwa na falsafa ya utu na usawa ilielekeza dhima ya vyombo vya habari nchini. Lengo pia lilikuwa kuhakikisha vyombo vya habari vinaunga mkono falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Kwa muhtasari, dhima ya vyombo vya habari katika kipindi hicho ilikuwa: (i) kuhabarisha wananchi kuhusu masuala yote muhimu ya ndani na nje ya nchi; (ii) kuelimisha, kufunza; (iii) kuwa kiungo cha mawasiliano ya serikali kwa wananchi; (iv) kuhamasisha wananchi katika masuala mbalimbali kama vile ukombozi wa majirani zetu waliokuwa chini ya ukoloni; (v) kukosoa kwa uhuru vitendo vyovyote vya viongozi wa chama au serikali ambavyo vinaenda kinyume cha misingi au maslahi ya nchi; (v) kuburudisha (rejea Ramaprasad 2001; Rioba 2009; 2012).
Baada ya uhuru pia serikali iliendelea kubaki na sheria zile zile za wakoloni za kudhibiti vyombo vya habari. Kwa mfano Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 au ile ya SHIHATA ya 1976, zote zililenga kudhibiti mfumo wa habari kwa namna ile ile wakoloni walivyokuwa wamefanya, japo kwa malengo tofauti.
Na hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikuwa na vifungu vilivyotambua au kulinda dhima ya vyombo vya habari katika jamii. Aidha, hata mwaka 1984, pale vifungu vya Haki za Binadamu vilipoingizwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977 bado vyombo vya habari havikutamkwa popote mbali tu na kifungu cha 18, kifungu kidogo cha (i) ambacho kilizungumzia haki ya kila mtu kuwa na maoni yake, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kukusanya, kupokea na kusambaza taarifa kupitia chombo chochote cha habari bila kujali mipaka na cha (ii) kilichosema: kila mtu anayo haki ya kuhabarishwa kuhusu masuala muhimu kwa maisha yake yanayotokea ndani na nje ya nchi.
Vyombo hivi kwa ujumla wake vilidhibitiwa na sera na sheria za vyombo vya habari, lakini pia na mfumo uliojengwa katika falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea na uliozingatia tunu za usawa, utu, umoja na uzalendo. Vyombo vya habari vilichukuliwa zaidi kama taasisi za kutoa huduma na si biashara ya kutafuta faida kama ilivyo leo.
Vyombo vya habari katika mfumo wa vyama vingi
Falsafa: Mawasiliano kujenga demokrasia
Baada ya matatizo ya kiuendeshaji, kisiasa na kiuchumi yaliyoikumba nchi, zikiwamo pia nchi nyingi za Afrika, katika miaka ya 1980, Tanzania iliamua kuridhia matakwa ya mashirika makubwa ya fedha duniani ya kurekebisha uchumi (Amani na wengine 2006, Malyamkono & Mason 2006).
Hata hivyo bado nchi ilikumbwa na msukumo mkubwa kutoka kwa baadhi ya wananchi waliotaka mabadiliko hasa kutokana na kushindwa kwa sera za kurekebisha uchumi za mashirika ya dunia ya kifedha (Chachage 1997). Kwa vile kwa wakati ule vyombo vyote vya habari vilidhibitiwa na serikali wananchi walihitaji uwanja huru zaidi wa kutolea mawazo yao.
Kwa mara ya kwanza yalianzishwa magazeti ya watu binafsi kama vile Fahari, Heko, Motomoto, Watu, Cheche, Radi na mengineyo ambayo yalijaribu kuziba ombwe la kihabari lililokuwa limesababishwa na ukiritimba wa sera, sheria na mfumo uliokuwapo.
Ni muhimu pia kubainisha hapa kwamba pamoja na kuwa vyombo binafsi vilivyoanzishwa vilianza kuandika habari na makala kali za kukosoa na kuumbua viongozi na mfumo, bado sheria zile zilizorithiwa toka ukoloni ziliendelea kutumika. Hata hivyo, kwa mara ya kwanza Watanzania walishuhudia vyombo vya habari vikiandika habari na makala kufichua mambo mbalimbali yakiwamo yaliyofanywa kwa kificho miaka ya nyuma (rejea Tegambwage 1990; Chachage 1997).
Kwa mara ya kwanza pia wananchi waliokuwa na mawazo tofauti na ya watawala walijitokeza na kueleza hisia zao, hasira zao na matarajio yao katika Tanzania ya demokrasia ya vyama vingi. Kufikia miaka ya 1990 tayari kulikuwa na vuguvugu kubwa la kutaka mabadiliko na tayari ilikwishaundwa kamati ya wananchi walioratibu mijadala ya kutaka kubadilisha mfumo. Kamati hiyo ilijulikana kama National Convention for Construction and Reform (NCCR) ambayo baadaye ilikuja kubadilishwa na kuwa chama cha siasa (NCCR-Mageuzi).
Hatua muhimu katika safari ya demokrasia ya vyama vingi ilikuwa pale Rais Mwinyi alipoteua Tume ya Jaji Mkuu Francis Nyalali kwa ajili ya kupata mawazo ya wananchi kuhusu aina ya mfumo wa uendeshaji nchi walioutaka. Tume ya Jaji Nyalali ilikamilisha kazi yake Februari, 1992 na kutoa mapendekezo kadhaa muhimu ikiwamo kufuta/na kurekebisha sheria 40 zilizoonekana kuwa kikwazo kwa demokrasia ya vyama vingi (rejea Ripoti ya Tume ya Nyalali 1992).
Pamoja na kuwa Tume ilibaini kwamba asilimia kubwa (77%) ya Watanzania walipendelea mfumo wa chama kimoja, bado walishauri mabadiliko au marekebisho makubwa ya kimfumo (Malyamkono & Mason 2006: 30). Mwaka huo huo 1992 kifungu cha 3 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilirekebishwa kuruhusu mfumo wa vyama vingi, huku marekebisho kama hayo yakifanyika pia katika Katiba ya Zanzibar.
Kwa muda mrefu, kwa mfano, kifungu cha 18 cha Katiba kiliendelea kueleza kwamba “bila kuathiri sheria za nchi, kila mtu ana uhuru wa kuwa na maoni...” Lakini mwaka 2005 baada ya harakati zisizokoma za wadau wa masuala ya uhuru wa habari, kifungu hicho kilirekebishwa na ile sentensi ya: “bila kuathiri sheria za nchi...” iliondolewa. Maana ya mabadiliko haya ni kwamba kwa sasa Katiba ina sauti ya juu kuliko sheria nyingine ndogo katika kulinda haki ya kila mtu kuwa na maoni au kukusanya, kupokea na kusambaza taarifa (rejea Tibanyendera 2012).
Hata hivyo, hadi sasa bado zipo sheria zinazokwaza uhuru wa vyombo vya habari ikiwamo Sheria ya Magazeti ya 1976 ambayo, pamoja na mambo mengine, inampa waziri mwenye dhamana ya masuala ya habari madaraka ya kufungia gazeti lolote wakati wowote anapoona inafaa kufanya hivyo.
Zimekuwapo juhudi zilizohusisha serikali, wadau wa habari na asasi za kijamii kuanzia mwaka 2001 kurekebisha sera ya habari na utangazaji ya mwaka 1993 ili ikidhi matakwa ya wakati. Hili lilikuwa zoezi la kwanza kwa serikali kushirikisha kikamilifu wadau wa habari na utangazaji katika kupata sera ambayo ilikuwa inakubalika kwa wote.
Sera hiyo ilikamilika mwaka 2003 na inajulikana kama Sera ya Habari na Utangazaji 2003. Baada ya kukamilika kwa Sera ya Habari na Utangazaji, mwaka 2006 serikali ilitaka kupeleka muswada wa Haki ya Kupata Habari kama ilivyoelekezwa katika sera mpya. Lakini wadau wa habari walipousoma muswada ule mtandaoni hawakukubaliana na maudhui yake (Rioba 2009).
Hivyo basi wadau wa habari MISA, Baraza la Habari Tanzania (MCT) na TAMWA wakakaa pamoja na kuanza mchakato mwingine wa kuwashirikisha wananchi ili kupata mawazo yao juu ya sheria hiyo ya habari. Wadau walimaliza kazi hiyo na kuandika mapendekezo ya miswada miwili na kuikabidhi serikalini.
Tokea mwaka 2009 mapendekezo ya wadau kuhusu muswada wa haki ya habari na huduma za vyombo vya habari yalipowasilishwa Wizara ya Habari, Utangazaji na Michezo yamekwamia pale, japo kila mara serikali huahidi itapeleka bungeni.
Kupitishwa kwa muswada huo kuwa sheria kungelimaanisha kufutwa kwa sheria mbaya kama ile ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo imekuwa ikitumika kufungia magazeti bila kufuata taratibu za kimahakama au hata kutoa sababu za kuridhisha kitaaluma.
Mkanganyiko unaojitokeza hapa ni kwamba serikali inaonyesha taswira ya kupenda kuendelea na sheria za demokrasia ya chama kimoja katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ambao unaamini sana katika uhuru wa maoni, kujieleza, kujua na uhuru wa vyombo vya habari kwa ujumla. Sura ifuatayo inajaribu kueleza kwa kina kidogo nadharia ya dhima ya vyombo vya habari katika demokrasia

src
Raia Mwema
Ayub Rioba
-