Thursday, March 27, 2014

Hivi kweli Serikali haiwezi kupambana na majangili?

Tuna vita mikononi mwetu hivyo ni muhimu tutumie kila tulichonacho kupambana na kushinda vita hiyo.

Vita hiyo ni ujangili ambao umekithiri nchini Tanzania, ambako vitisho vingi vimetolewa na viongozi wa ngazi mbalimbali za Serikali, lakini ujangili bado unaendelea kukithiri.

Majangili ni watu wa aina gani au ni maroboti? Ni lazima tuanze kujiuliza kwa kuwa haiwezekani wakawa binadamu wa kawaida ambao wanaweza kuishinda nguvu ya Serikali ambayo ina kila kitu cha kuweza kupambana nao.

Ripoti ya Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) iliyotolewa hivi karibuni inaeleza kuwa mwaka jana Tanzania ndiyo ilikuwa kinara au kitovu cha biashara ya meno ya tembo katika nchi za Afrika Mashariki.

Imeeleza kuwa takribani tembo 30 huuawa kila siku nchini na kufanya tembo 10,000 kuuawa kwa mwaka. Yaani tembo 30 huuawa kila siku na Serikali imekaa kimya ikipiga kelele kuwa itapambana na majangili kwa njia yoyote ile ili kukomesha tatizo hilo.
Serikali ina jeshi, ina polisi ina usalama wa taifa bado tembo 30 wanauawa kila siku na majangili ambao wamejengewa dhana kuwa wanaizidi “nguvu Serikali” na kufanya mauaji ya tembo na vifaru wakati wowote ule wanaojisikia.

Kwa jinsi hali ilivyo na inavyoendelea, inatia wasiwasi kuwa huenda majangili hao ni viongozi walioko Serikalini ambao hawawezi kudhibitiwa kwa njia yoyote ile au ndio wanaowalinda majangili kwa masilahi yao binafsi na familia zao. Nasema hivyo kwa kuwa ni aibu kwa Serikali kwenda kupiga domo Ulaya kuwa inapambana na ujangili nchini kwa nguvu zake zote, halafu tembo 30 wakawa wanaendelea kuuawa kila siku.

Haiwezekani majangili wakaua hata wale vifaru ambao Rais Kikwete aliwapata Afrika Kusini na kuwawekea ulinzi, halafu tukasema majangili ni watu wa kawaida.

Hapana! Hawa watu ni lazima watakuwa na mizizi mikubwa serikalini na kwenye vyombo vya usalama kiasi cha kuamua kufanya chochote, wakati wowote katika mbuga zetu za wanyama halafu kazi ya Serikali au wasimamizi wa mbuga iwe ni kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa majangili wameua tembo na kutoroka na meno yake.

Lazima kuna mkono wa mtu na ndiyo maana Wizara ya Maliasili na Utalii imefanya mabadiliko ya wakurugenzi hadi mawaziri, lakini bado ujangili unaendelea kukua kwa kasi badala ya kupungua
Idadi ya tembo nchini imeendelea kupungua miaka ya karibuni hasa katika pori la akiba la Selous ambalo lilikuwa na kiasi cha tembo 70,000 mwaka 2006, lakini idadi hiyo imeendelea kupungua hadi tembo 39,000 mwaka 2009 na hivi sasa pori hilo linao tembo 13,084.

Iadi ya tembo katika mbuga ya Ruaha nako imepungua kwa asilimia 44 toka 2006 na hivi sasa inakadiriwa ina tembo 20, 090.
Wakati hali ikiwa hivyo, nchini Kenya ujangili umepungua kutokana na ulinzi madhubuti na mkali uliowekwa katika mbuga zao, lakini nchi hiyo imekuwa ikitumika kama njia ya kusafirishia meno hayo kupitia bandari ya Mombasa ambayo majangili wanaipenda.

Interpol imeeleza kuwa pamoja na kwamba Uganda ni nchi ambayo haiko pembezoni mwa bahari, lakini imeanza kuwa ni njia ya kupitishia bidhaa hiyo hasa kutoka Tanzania.

Ni wakati sasa kazi ifanyike na siyo viongozi kupiga kelele kama wanampigia mbuzi gita.

gitaa huku tembo wakiendelea kuteketea kwa kasi ya ajabu.

bmeena810@gmail.com