Sababu ya wajumbe hao kugomea posho hiyo ambayo ni sh 300,000 kwa siku, wamedai ni ndogo, japokuwa hivi karibuni kiasi hicho kimelalamikiwa na baadhi ya wananchi, wakisema ni kikubwa kwa kuzingatia masilahi duni kwa makundi mengine kama walimu na wengineo.
Madai ya wajumbe hao yamefanya nipate shaka kama kweli watatimiza wajibu wao ipasavyo ili Watanzania wapate Katiba bora, kwani baadhi ya wajumbe wameonyesha wazi kutanguliza masilahi yao badala ya wananchi.
Kinachoshangaza ni kwamba, wajumbe hawa wameona jukumu hilo walilopewa na Watanzania kupitia taasisi zilizowapendekeza kama sehemu ya dili ambalo lingewasaidia kujikusanyia utajiri mkubwa.
Ikumbukwe hakuna mjumbe aliyelazimishwa kuingia katika Bunge la Katiba ila wao waliomba wenyewe kwa kiherehere chao na kusababisha kuwaamini kuwa wanafanya jambo hilo kwa manufaa ya kizazi kijacho, lakini kinyume chake wamewageuka.
Kwa wajumbe wanaoanza kuonyesha ulafi wa fedha mapema, wanakuwa wanatia shaka na kufanya nijiulize kama kweli kuna taasisi inayotaka mambo yao yapitishwe kwa kutumia rushwa kwa wajumbe hawa, hilo litashindikana.
Fedha wanayokataa sh 300,000, ndiyo mishahara wanayolipwa baadhi ya wafanyakazi wa serikali yetu kwa mwezi na bado kiasi hicho hawakipati kwa wakati.
Inasikitisha kuona wajumbe hao wanataka kuikwangua nchi hii maskini pamoja na kuwa na utajiri wa rasilimali lukuki huku ikielemewa na deni la taifa linalofikia sh trilioni 27.04.
Wajumbe hawa waliopo mjini Dodoma kwa niaba ya Watanzania zaidi ya mil. 45, wanasahau wapo baadhi ya walimu ambao hadi leo wanaidai serikali hii fedha zao.
Sidhani kama sababu yao ya wivu wa kijinga, kuwa wanastahili nyongeza ya posho hiyo kwa vile wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba walikuwa wakilipwa sh 500,000, inaingia akilini mwa wengi.
Wajumbe pengine wamesahau, tume ilikuwa na kazi ya kuandaa rasimu zote mbili ikiwamo kusafiri nchi nzima kutafuta maoni, tofauti na wao ambapo watakuwa wamejifungia sehemu moja tu.
Sina maana kuwa hawana kazi kubwa, kwamba kazi iliyobaki haiwezi kulinganishwa na ile ya Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba na wenzake.
Naamini, kama kweli taasisi zilizowapeleka wangejua wajumbe hawa wangegeuka kuwa fisi wa kutamani posho hata kabla ya kazi wasingethubutu kuleta majina yao.
Matarajio yangu, niliamini wajumbe hawa wangevutana katika hoja za marekebisho ya Katiba, suala lililowapeleka katika baraza hilo kwa masilahi ya wananchi, ningeona lina maana, lakini suala la posho, ambalo halikuwapeleka, kwangu nawaona kama wachumia tumbo.
Naamini serikali hii ya Rais Jakaya Kikwete inayojipambanua ni sikivu haitaweza kuongeza posho za wajumbe hao, hivyo kuifanya kazi hiyo kwa shingo upande, jambo linalonipa shaka kama Watanzania watapata Katiba bora.
Kumbe ni kazi ya wananchi sasa kufuatilia kwa makini na kujiandaa kwa ajili ya kuwapigia kura ya kutokuwa na imani nao, kama wahusika watashindwa kutimiza vema kilichowapeleka Dodoma.
Kama hilo la kura litafanikiwa kuwakataa, serikali itakuwa imepata hasara ya fedha za walipa kodi na kupoteza muda mwingi ambao haukuzaa matunda tuliyotarajia.
Waswahili wanasema: “Ukizoea kula nyama ya mtu, hautaweza kuacha.” Ndivyo ilivyotokea kwa Richard Ndassa, Mbunge wa Sumve (CCM), ambaye alifikisha hoja ya kuongeza posho kwa kisingizio kuwa wajumbe wanalalamika.
Kwa kuwa suala la kuomba nyongeza ya posho limekuwa ni mchezo ambao umekuwa ukipendwa sana na wabunge wetu, sasa wamejikuta wakiwaingiza hata wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba miguu yote bila wao kushtuka.
Napenda kumshauri Ndasa akumbuke kuwa bungeni pale hawapo kwa ajili ya posho, kama ni posho wanakula nyingi, na bado kuna miaka miwili imebaki, ataendelea kula ila kinachotakiwa kwa sasa ni kusimamia upatikanaji wa Katiba mpya.
Ni aibu kwa mbunge niliyekuwa nikimheshimu kama Ndasa aliyepewa ridhaa na wananchi kujipambanua kama mtu asiyejali masilahi ya taifa na badala yake, ameegemea kusaka fedha.
src
tanzanaia Daima