Saturday, February 15, 2014

Kujitoa ndani ya virusi vya kimfumo, anahitajika mtu

 
NAOMBA nichukue wakati wenu wa thamani kumpongeza Dk. Kitila Mkumbo kwa kuibua mjadala wenye tija kwa ajili ya kuliponya taifa na kuandaa mazingira rafiki kwa wale watakaokuwa na mtazamo mbadala.
Ni wasomi wachache wa kada yake wenye hulka iliyopevushwa kisomi kiasi cha kuwa tayari kuhimili mikikimikiki ya dhoruba kinzani kifikra. Kimsingi, nikiri, ni fikra zake ndizo zilizonipatia mahali pa kusimamia ili kujenga hoja zangu mbadala. Lakini pia katika muktadha huu, nafasi ya mhariri haiwezi kubezwa katika kufikia hitimisho hili.
Katika kuhitimisha mfulukizo wa makala haya, nipende kuweka bayana juu ya namna tunavyoweza kuanzisha mchakato wa kuweka miundombinu ya kufanikisha tiba ya matatizo yanayohandisiwa na mfumo wetu butu kimaadili ambao ndio ugonjwa unaoliangamiza taifa. Matatizo lukuki yanayojieneza kotekote mithili ya miguu ya pweza, chimbuko lake kuu, hapa nasisitiza, ni mdororo wa kimaadili.
Katika kufikia mustakabali mnono mniruhusu kutumia nukuu kutoka katika kijitabu cha Tujisahihishe, kama ngome imara ya ujenzi wa muktadha wa hitimisho la makala haya. Mwalimu Julius Nyerere anasema, nanukuu; “..daktari anayetoa tiba kwa tatizo asilolijua ni hatari sana kwa usalama wa afya ya mgonjwa.”
Tiba sahihi yapaswa kujijengea sifa turufu katika anga la bluu, lisilonyanyapaa gharama za utafiti huru ili kubaini kiini cha tatizo kwanza na kisha  tiba stahiki ifuate.
Nashukuru kwamba wasomaji wengi wamefikia kukubaliana na mtazamo wetu na Dk. Kitila juu ya ukweli kwamba vyama vya siasa CHADEMA na CCM vina gonjwa la mnyanyapao wa fikra mbadala, lakini, hadi sasa, tunatofautiana na Kitila juu ya kiini cha gonjwa lenyewe na tiba stahiki.  Hata hivyo kwa maoni yangu wagonjwa hawa wana viwango tofauti vya umahututi kimaadili. Naam, fikra yakinifu zitadai kuwa ipo tofauti ya hali ya wagonjwa. Lakini kwa ujumla wake, taifa zima linaumwa, na kwamba hali ya vyama hivi ni sampuli tu ya aina ya raia tulionao mijini na mavueni!
Tukianzia kuitathimini CCM, tunaweza kuifananisha na mgonjwa aliyepitia mikono ya madaktari wengi bila ya kupata nafuu. Madaktari waliomzunguka mgonjwa huyu wanaonekana kumkatia tamaa. Anapougulia na kutapatapa akipigania roho yake, wao wanampatia vidonge vya aspirini, tiba inayotuliza maumivu kwa muda lakini sio kuangamiza virusi msambao kimaadili. Lakini habari njema ni kuwa kati ya wagonjwa hawa wawili mmoja bado hajafikishwa ndani ya chumba hicho cha wagonjwa mahututi kimaadili! Je, atafika huko? Muda ndio utakaoamua.
Hata hivyo, kwa kuyatathimini mazingira ya Tanzania kisiasa, kiitikadi na kimaadili, binafsi, sishawishiki kuwekeza imani, kwamba mabadiliko  chanya yaweza kupatikana kupitia vyama vya siasa. Kwa mtazamo wangu sitokuwa tofautu na fisi anayesubiri msafiri adondoshe mkono wake! Kwa hiyo ili kujibu hoja juu ya nini kifanyike ili kulinusulu taifa hili,  itabidi kuwahamisha kidogo kutoka kwenye reli ya fikra mgando ya kutegemea michakato ya vyama vya siasa tu, kama  tiba pekee ya virusi vya kimfumo.
Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema, bila CCM imara taifa litayumba. Kauli hiyo yenye mwangwi mtamu ndani ya fikra za watawala ina viini nasaba vya nadharia ya ubwetesho, na hasa kama tutakipatia chama hadhi ya familia kubwa. Ni kauli ya jumla-jumla kiasi cha kumfanya rais, kama baba wa nyumba, kukwepa kuwajibika kama kiongozi mwenye dhamana kubwa kuliko watu wote katika taasisi husika. Ukweli ni kwamba bila ya kuwa na kiongozi imara katika nafasi ya urais taifa litayumba. CCM inayumba kwa sababu kiongozi wa juu siyo imara, na myumbo wa chama kinachotokana na kiongozi anayeyumba ndio kiini cha taifa kuyumba!
Ni kwamba, hata Nyerere, pamoja na kuwa na njozi bora ya Tanzania mpya, maono mapevu,  itikadi na falsafa inayokubaliana na hali ya mtanzania; pamoja na kuweka misingi bora ya ujenzi wa taifa kubwa, kwa maana ya kuwa na taifa lenye uwezo wa kujitegemea, alikosa misuli ya uthubutu wa kujenga  miundombinu imara kimaadili kwa ajili ya kutimiza njozi zake. Akiwa amezidiwa, naamini, na majukumu mengi kimataifa, wakati huo huo akiwa na hulka ya huruma, alishindwa kufanikisha mradi wa ujenzi wa chama chenye maadili na nidhamu ya hali ya juu, kitakachoendeleza maono yake hata kama akiondoka duniani.
Nifungue ukurasa mwingine mpya kwa mtazamo wenye ukakasi dhidi ya Unyerere, kwamba, udhaifu na mdororo wa CCM kimaadili katika kipindi cha Nyerere vilirutubishwa na hulka yake ya upole uliopitiliza, mabadiliko ya haraka kiuchumi yaliyosigana ki-urari na rasilimali watu wa kuziba ombwe lililotokana na mabadiliko hayo. Na zaidi, majukumu mengi kimataifa yaliyopelekea, yeye binafsi, kukosa utulivu wa kuwashughulikia watu wa nyumbani kwake! Kuhusu hulka ya huruma, Waswahili wanasema ukicheka na nyani utavuna mabua na ukicheza na mbwa utaingia naye msikitini!
Kwamba tunafuata itikadi ya kijamaa au kibebapari, ndiyo maana tumegonga mwamba, hiyo sio sababu, na wala kujiondoa kwenye mkwamo huu,   tiba sahihi si kuibeza na kujiondoa kwenye itikadi moja dhidi ya nyingine. Adui wetu mkubwa ni mdororo wa taifa kimaadili.  Tukumbuke kuwa, hakuna itikadi, iwe ya kibwanyenye au kijamaa inayoweza kuwanufaisha raia wake bila kuweka vipaumbele katika miundombinu imara kimaadili. Mwanafalsafa na mpembuzi wa masuala ya kisiasa ndani ya muktadha wa demokrasia, Alexis de Tocqueville(18o5-1859 , Mfaransa aliyefanya utafiti juu ya siri ya mafanikio ya taifa la Marekani, alihitimisha utafiti wake kwa maneno haya yenye mguso. “America is great because she is good, if America ceases to be good, America will cease to be great” Amerika ni taifa kubwa kwa sababu lina maadili. Litakapokoma kuwa na maadili litakama kuwa taifa kubwa. Huko ndiko taifa hili linakoelekea!
Ukweli  ni   kwamba ili kutoka hapa tulipo, iwe kupitia mlango wa kibepari au kijamaa, tunahitaji mtu mmoja tu atakayeifanya Tanzania  kuwa taifa kubwa. Mtu huyu si lazima atoke ndani ya chama chenye maono yake. Lakini ni lazima awe ni mtu mwenye uwezo kujitoa kafara kwa  kufanya maasi  dhidi ya mfumo  butu kimaadili uliomweka madarakani, na kisha kufungua ukurasa mpya wa ujenzi wa miundombinu kimaadili kwa ajili ya Tanzania mpya!  Haijalishi mtu huyo kwamba ametokea CHADEMA, CCM au ndani ya chama cha kufikirika cha rafiki yangu Kitilla. Muhimu hapa, taifa linahitaji mtu mmoja mwenye uwezo wa kufikiri na kutenda huku akiwa nje ya sanduku!
Rais mwenye misuli ya uthubutu, atakayeweza kusimamia mchakato wa mabadiliko bila kuogopa gharama ya kuchukua hatua hizo. Hatujapata kiongozi wa namna hiyo; kiongozi mwenye msimamo na ujasiri kama wa Robert Mugabe, lakini mwenye kiwango cha maadili kama cha Nyerere. Hatujapata mtu mwenye roho ya paka katika muktadha wa kushikilia maono yake kama ya Edward Lowassa, na mwenye uwezo wa kusimamia utekelezaji wake hata kama atachukiwa kama Paul Kagame, Edward Sokoine na Pombe Magufuli.
Kwa vile Katiba yetu imempa rais mamlaka iliyovuka mpaka, kuyumba kwa taifa hakuwezi kutenganishwa na  myumbo wa kiongozi wa juu kitaifa. Tatizo letu kuu kitaifa ni hilo, hatujapata mtu. Na mfumo unazuia una njia nyembamba kwa mtu wa kupatikana kwa mtu wa namna hiyo kupatikana. Tunahitaji kiongozi asiye mwathirika wa gonjwa la kupendwa na mataifa ya nje kwa gharama za raia wake; kiongozi atakayetumia karibu muda wote wa miaka kumi ya utawala wake ndani ya nchi hii ili kuliwekea taifa miundombinu imara kimaadili na kiuchumi, akitambua kuwa fursa zote za kulikwamua taifa hili ziko ndani ya nchi hii, na wala sio ughaibuni.
Naam, kiongozi atakayekuwa rafiki wa vyombo vya habari na kujenga mazingira ya kukosolewa na hata kuchukiwa kwa muda kitambo kabla ya wale wanaoongozwa kutambua upeo wa rais wao na kule anakowapeleka! Naam, rais mwenye kujiamini, na, asiye na  virusi vya kupendwa. Rais atakeyejiuliza maswali mazito kama ya mwandishi nguli, Jenerali Ulimwengu akihoji sababu ya taifa letu kupendwa na mataifa mengine. Rais, muumini wa kauli ya Elbert Hubberd aliyeandika hivi; “To avoid criticism, do nothing, say nothing, and be nothing,” kwamba ili kuepuka kukosolewa usifanye chochote, usiseme chochote na uwe si chochote.
Tunahitaji rais mwenye njozi pevu, ubunifu na uadilifu kama wa rais wa zamani taifa la Marekani hayati Ibraham Lincoln aliyewahi kusema, “akili pevu huchukia njia iliyopitiwa na watu wengi. Hutafuta maeneo ambayo hayajawahi vumbuliwa.” Kati ya mahitaji makubwa ya taifa letu ni kiongozi wa aina ya JF Kennedy aliyewahi kutamka, nanukuu “The problem of the world cannot possibly be solved by skeptics or cynics, whose hozons are limited by the obvious realities. We need men who can dream of thing that never were, and ask why not. Tafsiri isiyo rasmi, matatizo ya dunia hayawezi kutatuliwa na watu wenye mashakamashaka, ambao upeo wao wa kuona mbali unakomea kwenye mambo ya kawaida ya siku zote. Tunahitaji wanaoweza kuota yale ambayo hayajawahi kuwepo na kujiuliza; Kwa nini yasiwepo?
Wengi waweza kujiuliza mbona tumeingizwa kwenye anga la kufikirika? Tutapata wapi kiongozi wa namna hiyo. Kujibu swali hili bila kutoa mfano, ni sawa na kilihujumu. Mfano hai upo hapa jirani, taifa la Rwanda chini ya Paul Kagame. Kwa muda mfupi tu tangu taifa hili litoke kwenye msambaratiko vita vya wenyewe kwa wenyewe, Rais Kagame amefaulu kujenga miundombinu imara kimaadili, mshikamano wa jamii kitaifa na kuwafanya raia wake wamwamini na kumpa ushindi wa kishindo. Dunia imeanza kushuhudia jinsi nchi hii inavyopiga mbio kiuchumi kiasi cha kuyatetemesha mataifa ya magharibi.
Kwa mujibu wa The Transparency International Corruption Perceptions Index ya mwaka 2012, Rwanda ni nchi ya 50 katika orodha ya nchi 176 zinazopambana na rushwa; Uganda 130, Kenya  139, Burundi  165 na nchi yetu ilishika namba 102. Mwaka 2013 Bodi ya ushauri ya Umoja wa Afrika kuhusu masuala ya rushwa (African Union’s Advisory Board on Corruption) na Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa mataifa ya Afrika (UNECA) waliiteua nchi ya Rwanda kuwa mwenyeji wa mkutano wa mapambano dhidi ya rushwa. Mwenyekiti wa UNECA, Profesa Said Adejumobi, aliweka bayana kuwa Rwanda imechaguliwa kwa sababu ya rekodi yake ya kutoivumilia rushwa kwa kiwango cha asilimia sifuri.
Paul Kagame ana njozi za kulifanya taifa la Rwanda lisiwe tegemezi kiuchumi. Katika kufikia njozi hiyo tayari ameanzishwa mfuko Agaciro Fund utakaosaidia familia zote kutoka kwenye umaskini wa kutupwa na kuingia kwenye familia zenye vipato vya kati. Wakati taifa letu linaipiga teke teknolojia ya mawasiliano kwa kulifanya somo la kompyuta lisiwe sehemu ya masomo ya kupima ufaulu kwa kidato cha nne, Rwanda imelipa kipaumbele cha kwanza. Mpango huu mtambuka uko chini ya programu ya OLPC “One Laptop Per Children” ambapo kila mwanafunzi anagawiwa kompyuta mpakato moja bure.
Kagame anakusudia kulifanya taifa lake kwenda sambamba na kasi ya teknolojia ya habari na mawasiliano akiamini  kuwa habari sahihi ni muhimili wa mabadiliko ya jamii yoyote duniani. Si hivyo tu bali pia kutokana na msimamo wake imara, amelifanya Jiji la Kigali kuwa miongoni mwa miji bora duniani. Mji mkuu wa Rwanda, Kigali,  ndio mji wa kwanza Afrika kwa usafi, utulivu na usalama; Rwanda ni nchi ya tatu Afrika kwa ubora wa mazingira yake katika kuanzisha na kufanya biashara. Hayo yote ni matunda yanayotokana miundombinu imara kimaadili ambayo chimbuko lake kuu ni uongozi wenye uthubutu. Mara nyingi Kagame amewahi kunukuliwa akisema kuwa kutegemea misaada kutoka kwa wageni ni kumkufuru Mungu!
Tuhitimishe hivi; historia imehifadhi kwa uaminifu mkubwa rekodi za viongozi walioleta mapinduzi ndani ya nchi zao kutokana na kusimamia kwa uadilifu mkubwa kile walichokiamini kuwa ndiyo tiba ya matatizo yao. Mabadiliko, kamwe hayajawahi kuletwa na taasisi, iwe ni chama au dini, bali mtu au kundi la watu wachache ndani au nje ya chama wenye njozi, maono na mikakati yakinifu na uthubutu wa kufanya uamuzi mgumu lakini sahihi. Watu au mtu wa namna hiyo ndiyo mwenye uwezo wa kuwasha moto wa mabadiliko ndani ya jamii yetu iliyosambaratika kimaadili. Mtu huyo yuko wapi? Na ajitokeze.
source
Raia mwema

-