Wednesday, February 26, 2014

DIRA: Matumaini ya kupata Katiba bora yanatoweka



 
Na Elias Msuya,Mwananchi

Licha ya mchakato wa Katiba Mpya kuendelea kama ratiba na sheria inavyoelekeza, kuna dalili za kutopata Katiba bora yenye matakwa ya wananchi.

Ni kweli, tangu wazo la kuandikwa kwa Katiba Mpya lilipotolewa na kuanza kutekelezwa miaka miwili iliyopita, kumekuwa na michakato ambayo imekuwa ikiendelea mingine bila nia njema.

Kwa mfano, maoni ya wananchi yalikusanywa, kuchambuliwa,  kisha Rasmu ya Kwanza ya Katiba Mpya ikatolewa.

Baada ya hapo mabaraza yaliundwa ili kuichambua tena rasimu hiyo hadi ilipoundwa Rasimu ya Pili iliyopelekwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba ambalo limeanza kazi mjini Dodoma.

Kwanza, kumekuwa na mivutano mingi kuhusu suala la Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar na hilo lilitokana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba kupendekeza Serikali, tatu kulingana na uzito wa maoni ya wananchi, siyo idadi.
Hata hivyo,  hilo limeonekana kukichanganya chama tawala, CCM  kinachong’ang’ania Serikali mbili ingawa hadi sasa kuna baadhi ya wabunge wa chama hicho wanaonekana kupinga msimamo huo.

Kama wajumbe wa CCM walio wengi ndani ya Bunge hilo wakifanikiwa katika msimamo huo, ni wazi kwamba watapindua uzito wa maoni ya wananchi kwa mujibu wa Tume ya Katiba.

Pili, kuna utata unaoendelea katika tafsiri za Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Kifungu cha 25 (2)cha sheria hiyo kinaeleza majukumu ya Bunge Maalum la Katiba kuwa ni; “Litakuwa na jukumu la kuijadili rasimu ya Katiba na kuipitisha.”

Kwa maana hiyo, sheria hiyo inalifunga Bunge Maalumu la Katiba kuishia kujadili na kupitisha rasimu hiyo bila kuondoa neno wala kuongeza neno litakalobadili. Sheria hiyo hiyo kwa Kiingereza unatafsiri inayotoa  ruhusa kwa Bunge la Katiba, kujadili, kuondoa kifungu, kutunga kifungu ama kuiondoa na kuifuta kabisa rasimu iliyopo ambayo ndiyo maoni ya umma. Utata mwingine upo kwenye kanuni za uendeshaji wa Bunge hilo; kanuni ya 48 inayosema kutakuwa na faragha katika baadhi ya mijadala. ‘48(1) Kwa kuzingatia mazingira ya mjadala unavyoendelea ndani ya Bunge Maalumu, mwenyekiti wa anaweza kuamua mjadala husika uendeshwe katika kikao cha faragha cha Bunge Maalumu’. Faragha hii ni ya nini?
Hivi ni baadhi tu ya vifungu vyenye utata wa kisheria na vinaweza kutumiwa na wanasiasa au wajumbe wenye matamanio yao kupindisha matakwa ya wananchi.

Achilia mbali zile kelele za posho ambazo hata hivyo zimegonga mwamba, inaonyesha wazi kuwa wajumbe wengi wa Bunge hilo wametawaliwa na ubinafsi.
Wapo  waliotawaliwa na matamanio ya vyama, wengine makundi yao, yawe ya kidini, asasi za kiraia na mengineyo.

Kwa kuwa bado ni mapema, viongozi wa Bunge hili sasa wanapaswa kuangalia utata huu. Pia, wanapaswa kutawaliwa na uzalendo