Rais Jakaya Kikwete ametakiwa kufuta kauli yake ya kuwataka wana CCM kuacha unyonge na kujibu mapigo dhidi ya upinzani na ametakiwa kuomba radhi ndani ya siku tatu, vinginevyo suala hilo litafikishwa jumuiya za kimataifa.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo wakati wa kufunga Mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho Mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo Chadema wanaitafsiri kama kielelezo cha kuvuruga amani ndani ya nchi.
Kwa majibu CCM kupitia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kamwe hawatafanya hivyo.
“Kauli aliyoitoa Rais Kikwete ni ndogo na kutokana na vitendo vinavyofanywa na viongozi na wanachama wa Chadema kuvuruga amani nchini,” alisema na kuongeza kuwa dawa ya moto ni moto.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Operesheni wa Chadema, Benson Kigaila alisema kuwa Rais Kikwete anatakiwa kufuta alichokizungumza ndani ya siku tatu kuanzia jana, vinginevyo watalifikisha suala hilo mbele ya jumuiya ya kimataifa kama sehemu ya malalamiko yao.
Alisema kuwa Rais Kikwete ni Amiri Jeshi Mkuu, na alihoji kwanini awatake WanaCCM kujibu mapigo dhidi ya wapinzani badala ya kuacha hatua za kisheria zikafuatwa kwa kutumia vyombo husika ambavyo ni polisi na majeshi na mahakama.
Wakati huo huo, Nnauye alisema Rais Jakaya Kikwete hatafuta kauli ya kutaka wanachama wa chama hicho kuacha unyonge katika vurugu zinazofanywa na vyama vingine katika uchaguzi mbalimbali bali ataongeza nguvu.
Pia alisema Chadema haina adabu kwa kumpa Rais siku tatu aombe radhi kwani alitoa kauli hiyo kutokana na matendo inayofanya. Alidai katika uchaguzi uliopita wa madiwani, viongozi na wanachama wa Chadema walifanya vitendo vya kinyama dhidi ya wana CCM wakitumia silaha kama mapanga, visu, bisibisi na marungu.
Nape alionya kutohamasisha mapambano katika uchaguzi mdogo, kwani vitendo vilivyofanyika katika uchaguzi wa udiwani pekee vinatisha na kama ndivyo itakuwaje katika uchaguzi mkuu. Alisisitiza kuwa CCM inapeleka vijana wake Kalenga ili kujilinda na matendo kama hayo.
“Hatujawahi kuwa na makundi kwa ajili ya kupiga watu bali kujilinda na watu wetu na wapiga kura kwani Chadema hawataki siasa za kistaarabu,” alisema.
Chanzo: Mwananchi na Habari leo.
Wednesday, February 19, 2014
Home »
» CHADEMA watoa siku tatu kwa Rais Kikwete. Nape asema Rais hatafuta kauli bali ataongeza nguvu
CHADEMA watoa siku tatu kwa Rais Kikwete. Nape asema Rais hatafuta kauli bali ataongeza nguvu
2:42 AM