Thursday, February 20, 2014

Bunge la Katiba lisipobadilika halitafika




 

                              

                                 

            Bunge la katiba likiendelea mjini Dodoma 
Tunalazimika leo kutoa hadhari kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuwa, iwapo wataendelea kufanya vitimbi na vitendo vya kulidhalilisha Bunge wakati wanapokuwa wakitoa hoja zao kama walivyofanya juzi wakati Bunge hilo lilipokaa kumchagua mwenyekiti wake wa muda, taswira ya chombo hicho kilichoundwa kutunga Katiba Mpya itaharibika na malengo yake hayatafikiwa.

Wahenga waliposema siku njema huonekana asubuhi walikuwa sahihi kabisa kwa sababu jambo lolote linaloanza vyema huwa na uwezekano mkubwa wa kumalizika kwa mafanikio. Katika muktadha huo, Bunge linapoanza shughuli zake kwa kutawaliwa na zogo na vituko kama ilivyotokea juzi mjini Dodoma haliwezi kamwe kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Inawezekana kabisa kwamba wapo watu wanaoweza kusema kwamba matukio ya juzi bungeni yalikuwa madogo na kwamba yalitokea kutokana na kutokuwapo kanuni au mwongozo wa kusimamia uchaguzi huo wa mwenyekiti wa muda. Tunaweza kukubaliana kiasi fulani na hoja ya pili ya kutokuwapo kanuni na mwongozo, lakini hatuwezi kukubali hata kidogo hoja ya kwamba matukio hayo yalikuwa madogo, kwani yalivuruga mwenendo wa kikao husika, ambapo baadhi ya wajumbe walitoa kauli za kuudhi na kutumia lugha isiyo ya kibunge.

Vituko ndani ya Bunge hilo vilianza wakati wajumbe walipoingia ukumbini juzi jioni kupiga kura kumpata mwenyekiti wa muda baada ya wajumbe watatu waliogombea nafasi hiyo kujieleza na kujibu maswali ya wajumbe.

Baadhi yao waliuliza maswali yaliyoashiria shari na yasiyokuwa na tija kwa ufanisi wa mchakato huo. Kwa mshangao mkubwa wa wajumbe, mmoja wa wajumbe alimuuliza mmoja wa wagombea iwapo angefurahi kama angempigia kura.

Hatua ya kupiga kura ilizua utata mkubwa kiasi cha kusababisha uchaguzi kurudiwa. Hali hiyo ilisababishwa na tukio lililoonekana kwa baadhi ya wajumbe kama uchakachuaji wa kura, kwani idadi ya wajumbe waliopiga kura ilizidi idadi ya wajumbe waliopaswa kupiga kura.

Utata huo wa upigaji kura ulijenga hisia hasi kwamba upigaji kura katika vikao vijavyo vya Bunge hilo, ambapo baadhi ya mambo yataamuliwa kwa kupiga kura utachakachuliwa. Katika mazingira hayo, tutegemee nini kama siyo vurugu zitakazosababishwa na uchakachuaji wa kura?

Sisi tunadhani kwamba kazi kubwa itakayoukabili uongozi wa Bunge ni kutekeleza majukumu yake kwa uwazi, kutenda haki kwa wajumbe wote ili kuweka mazingira ya kuaminiana.

Tumesisitiza mara nyingi kwamba Bunge hilo litasambaratika iwapo litaendeshwa kwa ubabe na misingi ya itikadi za vyama badala ya kusimamia matakwa na maoni ya wananchi waliyoyatoa kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba.

Pamoja na baadhi ya vyama vya siasa, hasa CCM kuwalazimisha wajumbe wake walio katika Bunge hilo kufuata msimamo wake kuhusu vipengele mbalimbali vilivyo katika Rasimu ya Katiba, baadhi ya wajumbe hao wamesema wataweka mbele masilahi ya wananchi badala ya misimamo ya vyama vyao.

Kinachoshangaza ni kwamba kila mtu anazungumzia utaifa. Lakini likija suala hili la Katiba Mpya wengi wanajikita katika misimamo ya kisiasa.

Kikao cha Bunge hilo juzi kimetufumbua macho na kutambua kwamba wajumbe wake wasipojitambua na kujitayarisha kisaikolojia kuhusu uzito wa majukumu yao, upatikanaji wa demokrasia kupitia Katiba Mpya utabakia kuwa ndoto ya mchana.