Monday, March 3, 2014

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Profesa Ibrahim Lipumba, amewatahadharisha wajumbe wasitunge katiba ya kuwafurahisha wapigakura wao.
Pia amewataka wajumbe wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) , kutotumia wingi wao katika kupitisha katiba hiyo na badala yake watangulize masilahi ya nchi.
Profesa Lipumba (pichani) alitoa rai hiyo wiki iliyopita alipokuwa akichangia mawazo yake katika semina ya kujadili mapendekezo ya rasimu za kanuni zitakazotumika kuendeshea Bunge hilo lenye wajumbe 629.
“Naomba uzalendo utuongoze na tukumbuke hotuba ya Rais (Jakaya Kikwete) wakati anapokea Rasimu hii, alitutaka tuweke mbele masilahi ya nchi. Tusitegemee wingi wa namba,” alisema.
Profesa Lipumba aliongeza kusema “Unapokuja kwenye kutunga katiba unakuja kutunga katiba ya miaka 50 au miaka 100. Kwa hiyo isiwe katiba ya kufurahisha wapiga kura wako, Unapaswa kutazama kizazi kijacho”.
Mjumbe huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), aliwasihi wajumbe kutoa mawazo yatakayotoa katiba ya muda mrefu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Alisema wakati Ufaransa ikiandaa katiba yake baada ya mapinduzi, ilijiwekea masharti kwamba mjumbe yeyote atakayeshiriki katika kutunga katiba, asiruhusiwe kugombea nafasi yoyote ya uongozi.
“Lengo lilikuwa wapate fursa ya kutazama masilahi ya nchi tu badala ya kuangalia masilahi yao,” alisema.
Alisema katika mazingira ya Bunge hilo, wasidanganyike kwani kura ya siri ndiyo itakayowapatia Watanzania katiba bora.
src
mwananchi